HATIMAYE
ndoto za Mtanzania Mbwana Ally Samatta kucheza michuano ya Europa
League mwakani zimetimia leo, baada ya timu yake KRC Genk kufuzu
kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Sporting Charleroi Uwanja wa
Cristal Arena, Genk.
Kwa matokeo hayo, KRC Genk inafuzu Europa League kwa ushindi wa jumla wa 5-3, baada ya Ijumaa kufungwa 2-0 ugenini katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania nafasi ya mwisho ya Europa League nchini Ubelgiji.
Na Samatta leo alikuwa ana mchango wake katika tiketi ya Europa League kwa KRC Genk, alifunga bao moja na kusababisha penalti huku akicheza kwa kiwango cha juu.
Samatta (katikati) na wachezaji wenzake wa KRC Genk leo wamehitimisha msimu wao kwa kufuzu Europa League |
Samatta amefunga bao la pili dakika ya 27, lakini shujaa wa Genk leo alikuwa ni mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis aliyefunga mabao matatu, moja kwa penalti dakika ya 20 baada ya Samatta kuangusgwa na mengine dakika ya 56 na 71.
Bao lingine KRC Genk leo limefungwa na Sandy Walsh dakika ya 45 na ushei, wakati bao pekee la Sporting Charleroi limefungwa na Jeremy Perbet dakika ya 40.
Na baada ya kazi yake nzuri, Samatta akapumzishwa dakika ya 89 akimpisha kiungo Mghana, Bennard Yao Kumordzi.
Sporting Charleroi walimaliza pungufu baada ya mchezaji wao, Amara Baby aliyeingia kuchukua nafasi ya Mfaransa mwenzake, Clement Tainmont dakika ya 76 kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90 na ushei.
Samatta leo amecheza mechi ya 18 tangu ajiunge na Genk akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe pamoja na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
Katike mechi hizo, ambazo 10 ameanza, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, amefunga mabao matano, moja katika kila mechi Genk ikishindia 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem, 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende, 3-2 dhidi ya Club Brugge na 4-1 dhidi ya Sporting Charleroi leo.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.