YANGA YATUMA JINA LA CHIRWA CAF, APAA KUIFUATA TIMU ALGERIA


KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa amendoka Alfajiri ya leo kwenda Algeria kuungana na timu yake mpya, Yanga SC baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili jana.

Chirwa aliwasili jioni ya jana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na muda mfupi baadaye akasaini Mkataba wa miaka miwili.

Mara moja Yanga ilituma jina lake makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika siku ya mwisho ya usajili mdogo wa mashindano ya Afrika.

Yanga wanatarajia kupata leseni yake na CAF kuanzia leo jioni ili kukamilisha idadi ya wachezaji watano wapya, baada ya wazawa kipa Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Andrew Vincent na kiungo Juma Mahadhi.
Chirwa (katikati) akisaini. Kulia ni Wakili Jacqueline Majule na kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Isaac Chanji
Chirwa alikuwa mshambuliaji pacha wa Donald Ngoma katika klabu ya FC Platinums ya Zimbabwe.

Na baada ya Ngoma kuhamia Yanga, akawashauri viongozi wa timu hiyo wamchukue winga huyo wa kulia wa timu ya vijana ya Zambia chini ya umri wa miaka 23. 

Na inaaminika Yanga imetoa zaidi ya dola za Kimarekani 100 000 kuipata saini ya Chirwa ambaye anatokea FC Platinum ya Zimbabwe, klabu waliyotokea wachezaji wake wengine, Wazimbabwe Thabani Kamsuoko na Ngoma.

Mwaka jana, Chirwa alikataa kujiunga na Hobro IK ya Denmark baada ya kufuzu majaribio kutokana na kutoridhishwa na malipo - na maana yake Yanga itakuwa imempa mshahara mzuri.
Kikosi cha Yanga kiliwasili salama mjini Bejaia, Algeria mchana wa jana, tayari kwa mchezo fungua dimba wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Mouloudia Olympique Bejaia kesho.


Yanga imefikia katika hoteli ya kifahari ya Raya mjini humo na jana ilifanya mazoezi yake ya kwanza Uwanja wa jirani, wakati leo usiku itafanyia kwenye Uwanja wa Unite Maghrebine, utakaotumika kwa mchezo wa Jumapili.
Yanga iliwasili kutoka mjini Antalya, Uturuki ambako iliweka kambi katika hoteli ya Rui tangu Jumapili.

Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.

Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.

Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.

Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.

Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Chirwa anayewasili leo.
Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.

Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. 
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.