Na Saleh Ally
YANGA iko ikipambana katika mapambano ya michuano ya kimataifa kama ulivyoona jana katika mechi dhidi ya Medeama ya Ghana.
Mapambano hayo ya Yanga katika michuano ya kimataifa yanaweza kuwa na faida zaidi kiasi fulani kama maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Watani wao Simba, nao wanajiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Tena safari hii wakiwa wanataka kugeuza mambo kutokana na kuonekana Simba ya kawaida badala ya Simba ileee ya zamani ambayo ilikuwa inajulikana kwa ubora wa uchezaji ndani na nje ya nchi lakini suala la ubebaji wa makombe pia ndani na nje ya Tanzania.
Yanga na Simba zinataka kubadilika, zinataka kuwa bora na gumzo. Lakini zimekuwa zikikosea katika mambo mengi yanayoweza kuonekana ni madogo na hayana maana lakini ukweli ni hivi; yakifanyiwa kazi yatakuwa na faida sana.
Suala la jezi za Yanga na Simba, kila msimu unapokaribia kuanza utaziona timu hizo zikikabidhiwa zawadi ya jezi na mdhamini, mfano itakuwa ni kampuni ya bia ambayo inawapa mbele ya vyombo vya habari.
Jezi hizo, hukabidhiwa wakiwa pamoja na hapo ni mpango madhubuti wa mdhamini kujitangaza kutokana na suala hilo la kukabidhi jezi hadharani. Inawezekana linaweza kuendelea kwa kipindi kingine cha miaka 10 kama ukimya utatawala na wadau tukaendelea kukaa kimya.
Kampuni inayodhamini inataka kujitangaza kupitia kikao cha waandishi wa habari. Huenda miaka minne mitano lilikuwa ni jambo kubwa sana. Lakini kipindi hiki linazidi ‘kuzeeka’ na utamaduni au utaratibu huo unaonekana umepitwa na wakati kabisa.
Najua hakuna aliyeshituka, hakuna anayeona hauna tija, umepitwa na wakati na ikiwezekana kwa kuwa hauna ubunifu mpya basi hauna hata hiyo faida kwa mdhamini mwenyewe ambaye huenda naye ndani ya kitengo chake cha masoko licha ya kuwa kampuni kubwa, hakuna watu wabunifu pia.
Mfumo wa mambo unakwenda kwa ule utaratibu wa “kama ilivyozoeleka” na hakuna anayetaka kuumiza kichwa hata kidogo kwamba suala la kukabidhiana jezi kwenye mikutano ya waandishi wa habari kwa kipindi hiki ni “kichekesho chenye maumivu”, maana anayecheka atachukua muda mwingi akifanya hivyo hadi anaumia.
Simba na Yanga ni klabu kongwe, huu ni wakati wa kubadilika na kuepusha kuwaumiza wadau na utamaduni wao wa “vichekesho vyenye maumivu” na kuanza kufanya mambo ambayo ni sahihi.
Wadhamini wanaweza kujitangaza kwa njia nyingine ambazo ni bora, mfano kupiga picha zinazoonyesha wachezaji wakiwa na jezi mpya wanazitangaza kwa mara ya kwanza.
Kuna jezi za nyumbani na ugenini, wanaweza kupiga picha za jezi pekee za ugenini na baadaye za nyumbani pekee pia. Halafu wakachanganya zote. Lakini kukawa na picha za wachezaji tofauti na kuzifanya ni picha zenye mvuto ambazo rasmi zitaanza kutangaza jezi watakazozitumia msimu unaofuata.
Badala ya viongozi na wadhamini kuuza sura, bado inawezekana Yanga na Simba kutumia jezi pekee, kuzitangaza jezi zao mpya ikiwa ni pamoja na kuweka bei ya chini mashabiki wazinunue kwa wingi ili waweze kuzivaa kwa wingi wanapokwenda uwanjani kuwaunga mkono.
Ninaamini ubunifu ndiyo unaoifanya dunia kubadilika na kupiga hatua. Najua ni asilimia 15 tu hadi 20 ya watu ambao wamekuwa wakifanya ubunifu katika kila kitu kinachochangia mabadiliko ya dunia na wengine wanavutwa tu.
Lakini siamini ndani ya Yanga na Simba pamoja na wadhamini wao hakuna watu wachache wanaoweza kuwavuta wengine wakafanya mabadiliko na kufanya mambo ambayo ni sahihi kwa wakati tulionao.
Simba na Yanga, zilikuwa kitu kimoja kabla ya kutengana. Lakini ndiyo klabu zenye timu kongwe nchini zinazopaswa kuwa mfano na si kufanya mambo ya “kama ilivyozoeleka”. Badilikeni wakubwa.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.