Na Zaka Zakazi
Mei 22, 2016, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub Ally Upapa ‘Canavaro’ aliinua kwapa kupokea kombe la ubingwa wa Tanzania uliohesabiwa na shirikisho la soka hapa nchini TFF kama ubingwa wa 26 kwa timu hiyo kongwe zaidi hapa nchini kwa sasa.
Lakini ukiziacha rekodi za TFF, rekodi halisi zinaonesha kwamba Yanga siyo mabingwa mara 26 bali mara 25 kama itakavyodhihirika hapa chini
Ligi ya Tanzania ilianza 1965 na katika miaka mitatu ya kwanza, 1965-1967, Yanga ilisusia ligi katikati ya msimu na kuwaacha Sunderland na Cosmopolitan wakitoroka na ubingwa.
1968, kwa mara ya kwanza, Yanga ilishiriki ligi mpaka mwisho na hatimaye kuwa mabingwa. Ubingwa huo ukawapatia tiketi ya kucheza klabu bingwa Afrika 1968 na kufika robo fainali. Katika hatua hiyo, Yanga ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana kwa sheria ya kurusha shilingi baada ya sare ya 1-1 nyumbani na ugenini (wakati huo mikwaju ya penati ilikuwa haijaanza kutumika)
1969 Yanga walitetea ubingwa wao na kushiriki klabu bingwa 1970 na kutolewa tena kwenye robo fainali dhidi ya wale wale Asante Kotoko ya Ghana. Lakini safari hii mabao ya Kotoko yalitosha kwani licha ya sare ya 1-1 nyumbani, Yanga walifungwa 2-0 ugenini.
Itakumbukwa kwamba wakati huo, mpira ulikuwa katika zama za kati za ridhaa na wachezaji hawakuwa wakiutegemea kuendesha maisha yao. Wengi wa wachezaji, kama siyo wote, walikuwa wakifanya kazi kwenye makampuni, mashirika na taasisi mbalimbali huku mpira ambao ulikuwa ikichezwa zaidi na timu za mitaani, ukiwa kama sehemu ya kujifurahisha tu .
1970, ligi ya Tanzania ilikumbwa na mtikisiko mkubwa sana. Mwaka huo, FAT ilifungua milango zaidi kwa timu za mashirika na taasisi mbalimbali kama TPDF (Jeshi), Police, Magereza, na Cargo (bandari) kushiriki ligi.
Kuruhusiwa kwa timu hizi kukawalazimu wachezaji wa timu za mitaani kama Yanga, Sunderland na Cosmopolitan kuamua kuzitumikia timu za kazini kwao na kuziacha timu zao za mitaani.
Hali hiyo ikazifanya timu za mitaani zibaki pasi na wachezaji na hivyo kujitoa kwenye ligi zikisema hazina uwezo wa kuziba mapengo ya wachezaji hao.
Kutokana na hilo, FAT kwa kushauriana na chama cha soka cha Dar Es Saaam (Dar Es Salaam Football League Association DFLA) na kile cha mkoa wa Pwani (Coastal Region Football Association CRFA) ikaivunja ligi na kuiteua Yanga kushiriki klabu bingwa Afrika. Wakati huo, DFLA na CRFA ndizo zilizokuwa na nguvu kuliko hata FAT licha ya kwamba chama hicho ndicho kilikuwa cha kitaifa. Uamuzi huo ukapitishwa na BMT na kuwa rasmi.
Kwa maana hiyo Yanga ilishiriki klabu bingwa Afrika 1971 kama bingwa wa Tanzania 1970 ilhali mwaka huo ligi haikumalizika na bingwa halisi hakupatikana. Na huo ndiyo ubingwa unaoifanya Yanga iwe bingwa mara 26!
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.