Yanga imekiri kupokea barua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayowaelekeza kumlipa aliyekuwa kocha wao Ernie Brandts, klabu hiyo imesema itahakiki madai hayo kisha italipa pindi itakapojiridhisha.
Juzi TFF ilipokea barua kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) inayoelekeza Yanga kumlipa Brandts dola 11,000 (Sh milioni 24) baada ya kuvunja naye mkataba miaka miwili iliyopita.
TFF ilisema endapo Yanga haitamlipa Brandts raia wa Uholanzi mpaka wiki ijayo itakuwa katika hatari ya kupokonywa zake katika Ligi Kuu Bara.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, amesema: “Tumepokea taarifa za kutakiwa kumlipa Brandts, kwa kutambua umuhimu wa kuitikia agizo hilo, kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kufanya uhakiki wa kuona kama kweli hilo deni lipo, endapo tukikuta ni kweli basi tutafanya mchakato wa kulipa mara moja.
“Tunajua matatizo ambayo yatakuja kutukumba endapo tukikuta tuna deni halafu hatujalipa, kuna kupokonywa pointi au kushushwa daraja, hatutaki tufikie huko kipindi hiki ambacho tunawania ubingwa.
“Niwaambie tu mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi, tunafanya juhudi kubwa kuhakikisha hili tunaliweka sawa.”
Ikumbukwe kuwa, awali Kamati ya Hadhi ya Wachezaji ya Fifa iliiamuru Yanga kumlipa Brandts tangu Juni, 2015, lakini kutokana na kuchelewa kwao, imeamuriwa kulipa pamoja na asilimia tano ya deni hilo.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.