Na Ayoub Hinjo
Nahodha wa timu ya Simba, Mussa Hassan Mgosi amewatambia wapinzani kuwa msimu ujao wakae mbali kabisa na moto ambao utawashwa na timu hiyo yenye makazi yake Kariakoo, mtaa wa Msimbazi. Mgosi alisema “Najua mashabiki wetu wameumia sana na matokeo ambayo tulikuwa tunayapata mwishoni mwa ligi. Sisi wachezaji ndio wakulaumiwa kwa kushindwa kufanikisha hilo,naahidi msimu unaofuata hatutakuwa na masihara kama tuliyofanya msimu ulioisha”.
Nahodha huyo pia alielezea nafasi yake ilivyokuwa finyu katika kikosi cha kwana, “Kweli nafasi yangu kwenye kikosi ilikuwa finyu sana. Nilikuwa nacheza dakika chache mno,dakika 10 wakati mwingine dakika 5 na hata kama ikitokea nimeanza basi kipindi cha pili sirudi tena uwanjani.
Nachofanya sasa ni kujifua zaidi ili niweze kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Aliongeza tena “Unajua wakati mwingine inakuwa ngumu kumfanya Mwalimu abadili kikosi chache. Naamini katika kila program yake basi alikuwa anajua ni nani anafiti vyema siwezi kulaumu hilo kabisa sababu hata kama sikucheza majukumu yangu ya unahodha niliyafanya”
.
Akiongea kwa unyonge juu ya kushindwa kufunga magoli msimu huu “Mimi kama mshambuliaji nilisikitika sana kushindwa kufanya kazi yangu. Goli moja katika msimu nililofunga siwezi kujivunia nalo lakini kama nilivyoeleza hapo awali kuwa hata nafasi ya kucheza ambayo nilikuwa napata ilikuwa haitoshi”.
Akiendelea kuongea juu ya nafasi ya Ubingwa msimu ujao “Matatizo yetu si makubwa kama yanavyozungumzwa kwenye vyombo vya habari. Naamini matatizo hayo yakifanyiwa kazi msimu ujao tutapambana hadi mwisho na uhakika wa kuwa mabingwa kabisa tunao”.
Aliwasisitiza mashabiki wa Simba wasikate tamaa. “Mashabiki tumewakosea sana,kwa niaba ya wachezaji wenzangu naomba msamaha. Tunawaahidi mambo mazuri yatakuja msimu unaofuata. Wasichoke kutuunga mkono”. Alimaliza nahodha huyo.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.