NYOTA
wa Barcelona, Lionel Messi amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela na
kutozwa faini ya Pauni Milioni 1.7 kwa makosa ya kukwepa kulipa kodi.
Mahakama ya Hispania imemkuta na hatia ya makosa matatu ya ukwepaji kodi mchezaji huyo Muargentina mwenye umri wa miaka 29 pamoja na baba yake, Jorge.
Katika taarifa yake, Mahakama imesema kwamba hukumu yao inaweza kukatiwa rufaa Mahakaa Kuu ya nchi hiyo.
Pamoja na hayo, chini ya sheria za Hispania, mfungwa anayehukumiwa kifungo cha chini ya miaka miwili anaweza kuwa tu chini ya uangalizi, maana yake Messi na baba yake hawatakwenda jela.
Mahakama imemtaka Messi kulipa faini ya Pauni Milioni 1.7 na baba yake kulipa Euro Milioni 1.5 kwa uhalifu huo.
Mwezi uliopita Messi na baba yake walikana kufanya makosa na wote wakasema mchezaji huyo hakuwa anajua masuala ya kodi yaliyolifikisha suala hilo hapo.
Lakini Mahakama imekubaliana na Mwendesha Mashitaka wa Serikali kwamba Messi na baba yake walikuwa wana uelewa angalau kidogo wa masuala hayo nchini Hispania.
Maofisa wa kodi walisema kwamba walipata ushahidi kwamba baba yake Messi aliyatumia makampuni kama ya Uruguay, Uswisi na Belize kupunguza kodi katika mapato ya mchezaji huyo kutokana na haki za matumizi ya picha yake. Baba yake Messi alisema kwamba aliambiwa kwamba zoezi hilo lilikuwa halali.
Klabu yake, Barcelona imetoa taarifa ikisema kwamba itawasapiti Leo Messi na baba yake katika sakata hili.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.