Kama ilivyoripotiwa hapo awali, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kutoridhika na kujiridhisha kuwa mmoja wa wachezaji wa Jamhuri ya Congo-Brazzaville, alikiuka kanuni za mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, mwaka huu lilimkatia rufaa mchezaji Langa-Lesse Bercy katika Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Kutokana na rufaa hiyo dhidi ya mchezaji huyo wa Congo, Langa Lesse Bercy, CAF liliagiza apelekwe Makao Makuu ya Shirikisho hilo, lililoko Cairo, Misri kwa ajili ya kurudia na kuthibitisha umri wake kwa kipimo cha MRI (Magnetic Imaging Resonance).
TFF iliagizwa na CAF igharimie zoezi zima ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usafiri wa mchezaji husika na daktari wake pamoja na kulipia gharama za vipimo. TFF ilikubaliana na matakwa hayo ya CAF na kulipia.
Kipimo ilikuwa kifanyike leo Novemba 19, 2016 saa 5.00 asubuhi mjini Cairo, Misri. Ujumbe wa TFF wa watu wanne ukiambatana na madaktari wawili uliwasili mjini Cairo tangu Novemba 17, 2016 ili kuwa shuhuda wa zoezi la kipimo hicho.
Jana usiku saa 5.00 TFF ilipokea ujumbe kutoka CAF kuwa mchezaji Langa Bercy ameshindwa kusafiri kwenda Cairo kwa kuwa yuko katika eneo lililoko "vitani",eneo hilo halikutajwa.
TFF inaendelea kufuatia kwa karibu jambo hili ili kuhakikisha haki inatendeka .
Kadhalika Aidha TFF inaomba wadau wa mpira wa miguu wawe na subira katika kipindi hiki.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.