Uongozi
wa Yanga juzi Jumatatu kupitia kwa Makamu wake Mwenyekiti Clement Sanga
ulitangaza kuwa licha ya mabadiliko uliyoyafanya katika benchi lake la
ufundi, aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm
haondoki popote ila atakuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo na
nafasi yake itachukuliwa na Mzambia, George Lwandamina.
Kutokana
na hali hiyo, mshambuliaji wa kutumainiwa wa Yanga, Mrundi, Amissi
Tambwe amedai kuwa kitendo cha Pluijm kuamua kubaki klabuni hapo na
kusaidiana kazi na Lwandamina amekipokea kwa mikono miwili, hivyo
wapinzani wao watakoma.
Uongozi
wa Yanga ulifikia uamuzi huo wa kufanya mabadiliko hayo kwa lengo la
kuliongezea nguvu benchi lake la ufundi ili kuhakikisha timu hiyo
inatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara lakini pia iweze kufanya vizuri
katika michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo
itashiriki hapo mwakani.
Tambwe
amesema kuwa muunganiko wa makocha hao wawili katika benchi la ufundi
la timu hiyo, utaleta mapinduzi makubwa ndani ya timu katika kipindi
hiki ambacho inapambana kuhakikisha inatetea ubingwa wa ligi kuu.
“Baada
ya kuzipata taarifa hizo nimefurahi sana kwa sababu wote wawili ni
makocha wakubwa hapa Afrika, hivyo muunganiko wao utaleta mapinduzi
makubwa katika kikosi chetu.
“Lakini
pia hali hiyo itaongeza morali kwa sisi wachezaji katika harakati zetu
za kuhakikisha tunapambana vilivyo kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea
msimu huu, ukiachana na ubingwa wa ligi kuu lakini pia kufika mbali
kwenye michuano ya kimataifa,” alisema Tambwe ambaye kwa sasa yupo kwao
Burundi kwa mapumziko ambayo wachezaji wote wa timu hiyo walipewa baada
kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.