SIMBA SC imejirudisha jirani kabisa na mahasimu wao, Yanga SC katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 jioni ya leo dhidi ya wenyeji Maji Maji, Uwanja wa Maji Maji Songea mkoani Ruvuma.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 48 baada ya kucheza mechi 21, sasa wakizidiwa pointi moja na mabingwa watetezi, Yanga.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ahmed Kikumbo wa Doodma, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Ibrahim Salum Hajib Migomba dakika ya 19, hilo likiwa bao lake la nne msimu huu akiunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya winga Shiza Ramadhani Kichuya.
Katika kipindi hicho, Simba ilitawala vizuri mchezo na kama washambuliaji wake wangekuwa makini wangetoka wanaongoza kwa mabao zaidi.
Nafasi pekee nzuri ambayo Maji Maji waliipata wakashindwa kuitumia ilikuwa ni dakika 45 baada ya Marcel Bonaventura kupiga vizuri shuti la mpira wa adhabu, ambalo kipa wa Simba, Mghana, Daniel Agyei alitema mpira mbele ya Kevin Kibuta na Suleiman Kibuta, lakini wakashindwa kuurudisha nyavuni hadi ukaokolewa.
Kipindi cha pili, Simba ya kocha Mcameroon Joseph Marius Omog iliendelea kung’ara na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi, hivyo kuizima kabisa Maji Maji.
Kiungo mwenye kipaji kikubwa, Said Hamisi Ndemla aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 63 kwa shuti baada ya kona chini chini ya kiungo Mghana, James Kotei aliyetokea benchi kipindi cha pili.
Pamoja na kufungwa, Maji Maji walio chini ya kocha Muingereza mwenye asili ya Kongo aliyezaliwa Tanzania, Kali Ongala waliendelea kucheza vizuri wakitengeneza nafasi, lakini hazikuwa za maana.
Zikiwa zimesali dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho, mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 88 akimvisha kanzu beki baada ya pasi ya kichwa ya kiungo Mwinyi Kazimoto aliyetokea benchi.
Bao hilo liliimaliza kabisa Maji Maji na kutoka hapo wakawa wanacheza ili mechi iishe. Huu ni ushindi wa kwanza wa Simba katika Ligi Kuu mwaka huu, baada ya awali kutoa are bya 0-0 na Mtibwa Sugar na kufungwa 1-0 na Azam FC.
Kikosi cha Maji Maji kilikuwa; Hashim Mussa, Saleh Abdallah, Mpoki Mwakinyuke, Emmanuel Semwanza, Kennedy Kipepe, Alex Kondo, Iddi Kipwangile, Hassan Hamisi, Suleiman Kibuta/George Pole dk84, Marcel Bonaventure/Luka Kikoti dk73 na Kelvin Sabato.
Simba SC; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Novatus Lufunga, Method Mwanjali, Muzamil Yassin, Shiza Kichuya, Said Ndemla/Mwinyi Kazimoto dk76, Laudit Mavugo, Juma Liuzio/Pastory Athanas dk52 na Ibrahim Hajib/James Kotei dk59.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.