Kile kimuhemuhe cha hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Africa kilichokuwa kikisubiriwa kwa shauku kubwa hatimaye kimewadia. Sahau kuhusu Copa America achana na Euro na vurugu za Euro kule Ufaransa, lakini hii ndiyo game inayotuhusu sisi.
Tangu ilipotangazwa ratiba ya hatua ya makundi, mashabiki na wadau wengi wa soka walikuwa kwenye presha kubwa ya kuanza kwa hatua hii mithili ya kiongozi wa umma asiyeijua siku wala saa ya ukaguzi wa watumishi hewa ndani ya idara yake.
Hii ni wazi inatokana na kiu ya muda mrefu ya watanzania kushudia wawakilishi wao wakishiriki hatua hii yenye heshima kubwa tangu ilipotokea mwaka 2003 kwa mara ya mwisho. Na mechi ya ufunguzi wa kundi baina ya Mouloudia Olympique de Béjaïa (MöB) dhidi ya Yanga ni wazi utateka hisia za wengi hapo siku ya Jumapili. Na makala hii inakuletea uchambuzi wa kina juu ya vikosi, mifumo na mbinu zinazotegemewa na timu husika kuelekea katika mchezo huu wa muhimu.
Mfumo wa Mö Bejaia (3-5-2)
Tofauti na upenzi mkubwa wa timu za kiarabu kupendelea zaidi mifumo ya 4-4-2 na 4-1-3-2 ambayo huwafanya kucheza mpira wa moja kwa moja kwa kuwatawanya wachezaji kila sehemu ya uwanja, mfumo unaopendelewa zaidi na MöB ni 3-5-2.
Katika mfumo huu wa kutumia walinzi watatu wa kati kuanza pamoja mbele ya kisanduku cha golikipa na ma’wing-beki wawili kwenda kucheza juu kidogo ya mstari wa kati wa uwanja na kuongeza support ya umiliki mpira na upandishaji wa mipira kwenda kwa maforward wawili pale mbele.
Wakiwa katika mfumo huu inawafanya mabeki wao kukusanyika sehemu ya katikati ya goli wakitengeneza ukuta wao takribani mita 20 kutoka golini, hii inafanya kuwa vigumu kuwaingia kwa penetration passes kutokea kwenye sehemu ya midfield.
Udhaifu Unaojitokeza Kwenye Huu Mfumo
Kuna nafasi kubwa sana inayoachwa kuanzia katikati mwa uwanja mpaka sehemu ya pembezoni mwa box la MöB. Yanga ikifikisha mipira katikati mwa uwanja badala ya kulazimisha akina Niyonzima na Ngoma kuingia kwa nguvu ndani ya box, wanaweza kupiga pasi za kutanua uwanja kuelekea kwa ma winga ambao watakuwa na eneo kubwa la kusogea na mpira na kupata sekunde ya ziada katika kuwatafuta akina Tambwe na kuachia krosi murua ndani ya ‘sebule’ ya Mö Bejaia.
Vilevile kwa kutumia speed za akina Msuva wenyewe wanaweza kuanzisha counter-attacks na kusababisha magoli ya mwendo-kasi.
Style ya Uchezaji Wa Mo Bejaia
Kama zilivyo timu nyingi kutoka Kaskazini mwa Jangwa la Sahara, wachezaji wa MöB wana pumzi ya kiwango cha juu. Yanga itegemee mechi ya kasi kubwa na shinikizo la hali ya juu kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo mpaka kipyenga cha mwisho kutoka kwa mwamuzi Bouchaib El Ahrach kutoka Morocco.
Watu wa Kutazamwa Kwa Umakini
Unapokabiliana na timu yenye style ya soka la kushambulia mwanzo-mwisho ni vigumu kuweza kumuainisha mtu mmoja-mmoja kuwa ni hatari zaidi kwako, lakini kuna watu wawili wa kuwawekea umakini mkubwa, hasa wanapokaribia mita 30 kutoka langoni mwa Yanga.
1.) Mohamed Waliou Ndoye
Straika huyu raia wa Senegal anatambulika kwa uwezo wake mkubwa wa kupandisha timu kwa kasi. Magoli yake tisa ndani ya ligi ya Algeria manne ndani ya michuano ya Africa ni kielelezo cha makali ya straika huyu alienyakuliwa kwa saini ya €150,000 (Tsh Mill 300). Akitumia jezi namba 19 mgongoni mwake, Ndoye amekuwa sababu ya hekaheka kubwa langoni mwa wapinzani wa MöB iwe kwa kusababisha penalties au kuwafosi makipa wafanye makosa kwa kutumia mwili wake wa kibabe mithili ya Vicent Boussou na kupiga vichwa vizito kama Amis Tambwe. Utakuwa ushapata jibu nani wa kuvaana naye pindi mipira ya adhabu inapoelekezwa langoni kwa Yanga.
2.) Morgan Betorangal
Uwezo wake wa kuchanganya wapinzani kwa miguu yake yote miwili, ubunifu katika kukokota mipira, kuachia pasi za haraka na kuziomba tena sehemu ya mbele akiwa katika mwendo ni aina ya uchezaji unaomfanya Betorangal (Jezi #20) kuwa mchezaji hatari zaidi katika kuvuruga organization ya mabeki na kuwaweka mashabiki roho juu kwa muda wote wa mchezo.
Awali alikuwa alikuwa akitumika kama wing-back (aina ya uchezaji wa Bale alipotua Tottenham) kabla ya kuhamishwa nafasi na kusogea mahali pa juu na katikati zaidi ya uwanja, kisha kupewa uhuru wa kuufanyia mpira chochote anachokitaka pindi anapokaribia box la adui, hasa upande wa beki ya kulia.
Mzaliwa wa Ufaransa mwenye uraia wa Chad, Betorangal ni aina ya attacking-midfielder wa kisasa wanaoipa timu kitu cha ziada pindi mfumo wa mwalimu unapokwama kuleta matokeo chanya.
Kukimbiwa na Kocha Wao Mkuu
Wakati Yanga wakijizatiti na benchi lao la ufundi ambalo limekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu na wakipata muda wa kwenda kujifua kimaandalizi nchini Uturuki, mambo si shwari ndani ya kikosi cha MoB.
Kocha aliyekivusha kikosi katika hatua hii Abdelkader Amrani ‘babu’ alitangaza kujiengua katika nafasi yake huku akitarajiwa kujiunga na Etente Setif, wapinzani wao ndani ya Ligue 1 ya Algeria.
Hili ni pigo kubwa kwa timu kuweza kujiandaa chini ya kocha mpya na kuyafuata maelekezo yake katika wakati mfupi kabla ya mchezo mkubwa kama huu dhidi ya timu makini kama Yanga, iliyoupa mchezo huu umakini wa hali ya juu mno.
Yanga Inaweza Kupata Matokeo
Kumjua adui yako ni nusu ya safari ya ushindi, Yanga wana hii faida ya ziada baada ya kutumia wiki mbili za maandalizi kuelekea mchezo huu.
i./ Kuupoza Mpira Kwa Muda Mwingi
Kwa kuwa unakabiliana na mpinzani katika ngome yake kitu cha kwanza ni kuuharibu utaratibu wake wa maisha ya kila siku. Viungo wa Yanga wanatakiwa kuupozesha mpira kwa mtindo wa pasi fupi za kampa-kampa tena, na pindi itapowalazimu basi wapige pasi za haraka kuelekea mashavuni mwa box la MöB. Bejaia wanataka kuumiliki mchezo kwa zaidi ya 60%-70% na haitowapa pumzi akina Kamusoko kupigiana walau pasi tano kwa kuzibana njia zote za kupitishiana mipira.
ii./ Kuwalazamisha Mabeki wa Kati Wafanye Makosa
Utumiaji wa mabeki watatu katikati umesababisha makosa mengi zaidi langoni mwa Bejaia na kuwa chanzo kikubwa cha magoli wanayofungwa. Mawasiliano yanakatika pindi timu inapowashukia mabeki wao kwa kasi, na kujichanganya kwa mabeki na viungo wao kunaweza kabisa kuwatunuku Yanga magoli ya muhimu. Mlinzi wa mwisho Zidane Mebarakou (#5) ni mzito sana katika kunyumbulika, kwa kasi na nguvu za Donald Ngoma huu unaweza ukawa mpenyo.
iii./ Yapigwe Mashuti ya Nje Ya 18
Pamoja na pengo la Juma Abdul, lakini bado Yanga ina hazina kubwa ya wafumua mizinga. Mashuti kama lile la Mateo Anthony mita 35 dhidi ya Sagrada, na ufundi wa kumchungulia kipa kama aliouonesha Tambwe pale Sokoine mbele ya kipa mzoefu Juma Kaseja, zitakuwa silaha muhimu mno kwa Yanga.
iv./ Upangaji Mzuri Wa Ukuta Nyakati Za Faulo
Kwa level hii ya mashindano yalipofikia, Dida/Barthez hawatakiwi kufanya makosa yatakayopelekea kufungwa magoli yatokanayo na mipira ya adhabu (faulo/kona).
MöB wanawapigaji wazuri wa mipira iliyokufa wakiongozwa na fundi Faouzi Yaya (#10) aliyewafunga Zamalek kwa faulo ya mita 28. Upangaji wa ukuta na juhudi za kuruka na mtu ndio kitakachoziweka nyavu za Yanga mahali salama.
Nguvu ya Mashabiki Wa MöB “Ultras Saldae Kings”
Huu ni mhimili mwingine wenye msaada mkubwa katika mafanikio ya MöB. Pindi unapotia mguu wako ndani ya Stade de l’Unité Maghrébine utaweza hisi joto la hamasa inayotengenezwa na mashabiki wa timu mwenyeji ambao huanza shamrashamra zao kabla hata ya timu kuingia kufanya warm-ups. Sahau kuhusu mbeleko za waamuzi, The Saldae Kings ndio jeuri kuu ya MöB, hawa jamaa huugeuza uwanja mdogo wenye uwezo wa kuchukua watu 19,000 kuwa ngome yenye jeshi kubwa na kutimiza wajibu wa mashabiki kama mchezaji wa 12 kikamilifu katika kila dakika ya mchezo. Kwa uzoefu walio nao Yanga hadi hatua hii waliyoifikia hivi sasa naamini wamejizatiti kisaikolojia dhidi ya hali za mashabiki wenye wazimu kama hizi, nasi tukiwa na cha kujifunza vilevile hapa.
Mwishoni wa siku mfumo na style haziupi timu ushindi, bali jitihada na umakini wa 101% kwakila mchezaji aliyeaminiwa kuvaa jezi kutambua thamani ya kila sekunde inayomuweka uwanjani.
Tunawakubali, tunawaamini, tunajua mnaweza piganeni kiume katika usiku utakao kuwa mrefu mno kwa mamilioni ya watanzania tulio nyuma yenu.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.