Rais
wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) Ndugu Wallace Karia ametoa salamu
za pongezi kwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes) na ile ya chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa
kufuzu katika michezo yao iliyochezwa jana huko DR Congo na Burundi.
Ngorongoro
Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za
Africa za Vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba
baada ya ushindi wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90
kumalizika kwa sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa
kwanza uliochezwa nchini Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu
hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka
17 inayoendelea huko Burundi.
Rais
wa TFF Ndugu Karia amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni
faraja kubwa kwa Tanzania na inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea
kuwekeza kwenye soka la vijana.
Amesema
Vijana hao wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada
kubwa na wanastahili pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za
mabenchi ya ufundi ya timu hizo.
“Tumepokea
matokeo ya Vijana wetu wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa
kwasababu tumekuwa tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri
ambayo yanaonekana uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea
sifa kubwa Tanzania kwa ujumla” alisema Karia.
Aidha
Rais wa TFF Ndugu Karia amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia
maandalizi mazuri zaidi timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika
mashindano mbalimbali yanayowakabili.
Amesema
TFF inajivunia vijana hao ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba
watu mbalimbali, taasisi, makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na
kuiga mfano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na
kuisaidia Ngorongoro Heroes katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye
mchezo wa marudiano.
Amemalizia
kwa kuwashukuru wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira
wa Tanzania huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao
kwa TFF.
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.